Jumatatu, 27 Machi 2017

NAMNA YA KUPATA UHURU WA KIFEDHA KIBIBLIA

JIUNGE NA VIPAUMBELE KWANZA.



MAFANIKIO NI KUWA NA VIPAUMBELE BORA

* indicates required







Bwana Yesu apewe sifa!
Ndugu msomaji wa makala nazotoa kila wiki, nimesukumwa leo ndani yangu kukushirikisha kitu kifuatacho ambacho kila aliye wa Bwana anapaswa kuwa nacho katika moyo wake! Ni kweli kila mtu anatamani kuwa na fedha nyingi, lakini kuna swali huwa hatujiulizi, nalo ni hili: Nataka fedha nyingi kwa ajili ya nini? Hili ni swali zuri sana tunalopaswa kujiuliza kila wakati, kwa sababu unaweza ukawa unapata fedha kisha zinakujeruhi, kwani hujawi kusikia kuwa kuna ndoa zinakufa fedha zinapoongezeka? Kuna watu wanafikiri kuwa ukishakuwa na fedha, basi wewe ni mbarikiwa! Mimi nakataa usemi huu, kidunia ni usemi sawa, lakini Kibiblia au Kimungu si usemi sahihi hata kidogo. Kuna watu wakipata fedha, dhambi zinapata nafasi mioyoni mwao, na wengine mpaka zinawanjia heshima. Ndiyo maana ni muhimu, wale walio wa Bwana Yesu, tumtafute kwa bidii ili atawale mali zetu ndipo tutakuwa salama.
Uhuru wa kifedha ni nini Kibiblia?
Dondoo ya 1:
Ni wakati tabia ya moyo wako haitawaliwi na kuwepo au kutokuwepo kwa fedha bali itawaliwe na Roho Mtakatifu, katika neno la Mungu la Biblia.
     -Ukisoma Mathayo 6:21, maandiko yanatuambia mahali hazina (fedha) ya mtu ilipo, ndipo na moyo wa huyo mtu ulipo. Kwa mantiki hii, fedha ina nguvu kuliko moyo wa mtu. Na fedha ikiwa na nguvu kuliko moyo wako, bado hujawa na uhuru wa kifedha ule Mungu anaoutaka. Hivyo ni muhimu tukabidhi vyanzo vyetu vya fedha au mapato kwa Mungu kwa njia ya maombi, ili Roho Mtakatifu atawale nguvu iliyomo ndani ya fedha ili kuusaidia moyo wako usitawaliwe na fedha.

Dondoo ya 2:
Uhuru wa kifedha ni wakati unaweza kufanya chochote kile ambacho Mungu anataka ufanye bila kukwamishwa na kutokuwepo kwa fedha.
-Ni muhimu kwa watu wa Mungu kumtegemea Mungu katika mambo ambayo Mungu anataka wafanye. Una vitu vingapi moyoni mwako ambavyo unajua kabisa ya kuwa Mungu anataka uvifanye lakini kiwango cha fedha ulichonacho kinakukwamisha? Kwa mfano; semina za neno la Mungu, kujiendeleza kimasomo, kupanua biashara yako, au kubadilisha kazi ulinayo au kuchangia gharama za kazi ya Mungu katika kanisa au huduma mbalimbali.
    Umewahi kujiuliza nani huwa anaamua hayo mambo niliyoyataja hapo juu yatekelezwe vipi-ni moyo wako au fedha uliyonayo?
Kwa watu wengi kinachoamua ni fedha waliyonayo halafu mioyo yao inafuata uamuzi wa fedha zao!
Je! moyo wako una nguvu ya kuikataa fedha unayopewa kwa masharti yasiyo mazuri kama msaada au mkopo-na bado mipango yako ikatekelezeka na hali ya uhuru wako wa kiroho ukaendelea kuwa mzuri?

Dondoo ya 3:
Ni wakati mapato yako yanapokuwa ni makubwa kuliko mahitaji na matumizi yako ya kila siku-bila kudhoofisha hali yako ya kiroho. (Wafilipi 4:19)
"Na Mungu wangu atawajazeni kila mnakihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu".Njia mojawapo anayoitumia Mungu kukujaza na kila unachokihitaji ni fedha-maana imeandikwa, "......fedha huleta jawabu la mambo yote" (Mhubiri 10:19). Ikiwa na maana, Mungu anaweza kutumia fedha kujibu au kukupa jawabu la mahitaji yako.
Ikiwa ni hivi basi, uhuru wa kifedha kwako utakuwa pia na maana ya kuwa, Mungu anapotumia fedha kukupa jawabu la mahitaji yako, usihamishe imani yako toka kwa Mungu na kuiweka kwa fedha. Au usihamishe imani yako toka kwa Mungu na kuiweka kwenye kazi, mradi, kampuni, huduma, biashara, sadaka au mtu unayemtegemea sana bali imani yako ibaki kwa Mungu, haleluya!
Zipo maana nyingi za uhuru wa kifedha kibiblia, lakini hizi chache, zikupe changamoto ya kupanuka zaidi juu ya jambo hili. NB: Weka imani yako kwa Mungu uwe na fedha nyingi au kidogo. Fedha zinaweza kutumiwa na Mungu kukupa jawabu la hitaji lako, lakini Mungu apewe nafasi ya kwanza moyoni mwako.
Wiki ijayo tutaangalia njia za kibiblia zinazoweza kutusaidia kupata uhuru wa kifedha.
Mungu akubariki, mshirikishe na mwingine ujumbe huu! 

0 maoni:

Chapisha Maoni