Ijumaa, 24 Februari 2017

UMEJIAANDAJE KIUCHUMI MIAKA 5 IJAYO?

Ndugu msomaji wa VIPAUMBELE KWANZA umeamkaje siku ya leo? Ni matumaini yangu kuwa umeamka mapema kabisa na harakati za kupambana na maisha ya kila siku. Leo hii napenda nikushirikishe jambo moja muhimu. 
Je! umejiandaa vya kutosha kuishi katika mafanikio ya kiuchumi miaka 5 ijayo yaani 2023. Umejiwekea malengo gani ya kuhakikisha unakuwa na uchumi mzuri kufikia mwaka 2023? Siku moja nilimuuliza hili swali rafiki yangu nayefanya naye kazi mahali fulani akaniambia hivi, "Faustine huwezi kuweka malengo ya miaka mingi hivo, akaendelea kusema, "una uhakika gani kuwa mwaka 2023 utakuwa hai? Mimi kwanza nilimshangaa na nilishtuka sana, nilitegemea angeniambia, ondoa mashaka. Huu ndio ukweli halisi, watu wengi hasa vijana wa kizazi hiki, kweli wanatafuta fedha na wanapata, cha ajabu mno, wanazitumia ovyo hovyo, mwisho wa siku wanajikuta hawana kitu. Wengi wanajitahidi wananunua mashamba na viwanja ni vizuri sana. Lakini swali langu liko pale pale, wamejiandaaje kifedha miaka hiyo ijayo? Ndugu msomaji unayesoma makala hii, inawezekana umeshajijenga, Mungu akuinue zaidi, lakini pia inawezekana bado unapambana, ningekushauri ujitahidi kuwa na malengo mahususi ya kimkakati na yanayotekelezeka. Ili uweze kujiandaa vizuri fanya jambo hili moja tu kwanza.
ANZA KUWEKEZA FEDHA ZAKO KIDOGO KIDOGO .
Narudia tena anza kuwekeza fedha zako kidogo kidogo kwa watoao riba. Nina uhakika baada ya muda utaanza kuona mafanikio kwako. Ngoja nikupe mfano mzuri.
Kuna rafiki yangu mmoja alinitangulia kikazi, yeye alivyoanza kazi yake alipata bahati ya kuwa na siri hii muhimu. Akatafuta taasisi nzuri akawekeza fedha zake kwa miaka 5 tu. Alijinyima akaanza kuweka (deposit) Tsh.50,000 kila mwezi kwa miezi 60 au miaka 5. Akajikuta ana Tsh.499,645.19 ambayo ukikadiria ni karibu Sh.5, 000, 000. Akapata mtaji wa kuanzia biashara. Hivi leo tunavyoongea yuko mbali kimaisha. Unaweza ukasema, anafanya kazi, ni sawa, lakini ukipiga mahesabu yako vizuri utagundua kuwa, sh.50, 000 kwa mwezi ni sawa na sh.1300 kwa siku. Ubaya ni kwamba, vijana walio wengi siku hizi wanatumia fedha zao kwa fujo wakidhani kuwa wataendelea kuwa nazo. Si kweli usijidanganye, maisha yanabadilika, miili yetu inachoka. Ifike mahali fedha nazo zitufanyie kazi. Unataka kuniambia huwezi pata sh. 1000 tu kwa siku ukaiweka kando? Kama huwezi angalia unatumia shilingi ngapi kwenye vocha ya simu na mawasiliano kwa mwezi. Nakushauri jitahidi usiishi kama BOSS wakati bado hujafikia uhuru wa kutosha wa kifedha. Acha kutapanya pesa, kumbuka una wategemezi wengi hapo baadaye. Na kama tayari unao wategemezi, basi huna budi kutulia na kujipanga vema. 
Ndugu msomaji, mwaka juzi kuna kundi la watu 7 waliungana wakawa wanaungana kwa kuweka sh. 50,000 kila mwezi kila mmoja. Hivyo wanachanga sh.350, 000 na wameamua kufungua biashara fulani mwaka 2021, kwa mahesabu ya haraka hawatakosa mil.48. Hii ni nguvu ya uwekezaji. Nakutakia siku njema! 

Maoni 1 :