Jumamosi, 25 Februari 2017

VITU HIVI VINNE AMBAVYO HUNA BUDI KUWAFUNDISHA WATOTO WAKO

Habari za jioni ndugu msomaji! Pole kwa majukumu ya hapa na pale. Mshukuru Mungu kwa yote yaliyotukia yawe mazuri au mabaya.
Jioni napenda nikushirikishe jambo hili muhimu japo wengi wanaliona kama halina umuhimu. Jizoeze kuwafundisha au kuwapa maarifa watoto wako yatakayowasaidia siku za usoni. Sizungumzii elimu dunia iliyo katika mfumo rasmi, hapana nazungumzia maarifa. Watu wengi wanafikiri wataishi milele, na kwa sababu hiyo kuna baadhi ya vitu huwa wanavipuuzia katika maisha yao.

Katika jioni njema nakushauri jizoeze kukaa na watoto wako mara kwa mara, kama wako shule iwe day au boarding (bweni) bado watakuja nyumbani likizo! Kama wewe ni mfuatiliaji wa mambo utagundua kuwa watoto wetu wanahitaji kupata vitu hivi katika maisha yao! Ukifa haya mambo yatawasaidia sana, ndiyo maana haijalishi mtaacha mali nyingi kiasi gani, kama hawakuandaliwa uwe na uhakika mali zitaisha na hawatazifaidi kabisa. Ni mambo tunaona kila siku.

Mambo hayo ni:
1. Lazima watoto wako wafundishwe masuala ya fedha
2. Lazima wajifunze kompyuta ipasavyo
3. Lazima wawe na hofu ya Mungu maishani mwao.
 Kila upatapo mwanya wafundishe watoto wako mambo haya yatawasaidia sana pindi hampo. Hakuna atakayeishi milele, kila mwenye mwili hana budi atatoka katika dunia hii.

FEDHA ni nguzo ya muhimu sana kwa kila mtu kujifunza ili itumike ipasavyo.
Ni muhimu wanao wajue tabia za fedha na misingi yake, kwani jambo hili litawasaidia. Jambo hili sio OPTIONAL (si la kuamua uchague au usichague), ni lazima wajifunze vema. Fedha zimeangamiza wengi sana hata watu wazima tena wenye elimu. Kibaya zaidi hiki kitu cha fedha, hutakikuta kwenye SYLABUS ya mfumo wa elimu wa nchi yetu. Kuna watu ni maskini kwa kuwa tu walikosa kujua TABIA ZA FEDHA. Usiishie tu kuwapeleka shule ukadhani umemaliza, wafundishe kila wakati. Kwa mfano, jizoeze kuwapa hela za matumizi na baadaye waulize wamezitumiaje. Wafundishe kujua vitu ambavyo ni VIPAUMBELE kwao na VILE ambavyo sio VIPAUMBELE kwao. Watu wengi wamefaulu kuweza kutafuta fedha, wengi wanakwama kwa kuwa hawajui namna ya kukaa nazo hizo fedha. Siku moja nilikuwa namfundisha mdogo wangu namna ya kukaa na fedha kwa nidhamu, nikamuambia hivi, siku zote, ukipata fedha iwe ndogo au kubwa lazima kabla ya matumizi, atoe FUNGU LA KUMI, baada ya fungu la kumi, ajilipe yeye au aweke AKIBA. Baada ya akiba, atenge kiasi cha KUWEKEZA. Na pesa itakayobaki iwe ni MATUMIZI YALIYO LAZIMA. Mfundishe mengi hatua kwa hatua, hatakusahau. Mpaka hivi tunavyoongea, mdogo wangu ananishukuru kwa jambo hili.

KUJUA KOMPYUTA SI UCHAGUZI
Siku tulizo nazo ni za TEKINOLOJIA (technology), hivyo awe amepata elimu dunia au awe hajapata elimu dunia, lazima mtoto katika nyakati hizi ajue kutumia kompyuta. Awe maskini au awe tajiri, computer lazima ajifunze...
Tutafiki wakati mambo mengi tunayoyaona leo yakifanyika kikawaida yatakuwa kitekinolojia zaidi. Uwe mfanyabiashara mdogo au mkubwa na hujapata elimu dunia, lazima ujifunze na wewe kutumia computer na pia lazima wanao wajue kutumia hiki kifaa muhimu cha kielektroniki. Miaka mingi iliyo mbele yetu utajua jambo hili ninalokueleza. Nakuomba uyafanyie kazi.

KUWA NA HOFU YA MUNGU
Ewe mzazi wa kizazi hiki nadhani huhitaji kushawishiwa kumlea mwanao katika njia impasayo ili baadaye awe baraka kwa jamii na kwa dunia. Siku hizi kuna mambo mengi yanayojitokeza tena mengine yanakubaliwa kisheria, hivyo watoto wetu tuliopewa tuhakikishe tunawapa malezi bora kila wakati. Siku hizi kuna USHOGA, na mambo yanayofanana na hayo, tujitahidi kuwaonya kwa huzuni na kwa uchungu, huku tukiwaeleza mabaya haya lakini la muhimu zaidi kuwafundisha kumjua Mungu na kumtumikia yeye. Tukipoteza watoto tumepoteza jamii na ulimwengu. Watoto wetu wanazaliwa katika nyakati hizi mbaya. Mungu awe nawe, nakutakia jioni njema. Wako VIPAUMBELEKWANZA master!
 

Maoni 1 :

  1. Lucky Club Casino Site Review
    Lucky Club luckyclub.live is a trusted, trusted online casino and sportsbook that is part of the Sportsbook and Casino. Read all about the games, bonuses,  Rating: 2 · ‎Review by Lucky Club · ‎UK Players

    JibuFuta