Jumatatu, 20 Februari 2017

MAAMUZI UNAYOCHUKUA JUU YA PESA UNAZOPATA YANAWEZA KUKUFANYA UWE TAJIRI AU MASKINI

Ndugu msomaji wa VIPAUMBELE KWANZA habari za mchana? Binafsi namshukuru Mungu sijambo!
Mchana huu naomba tuzungumzie jambo moja kubwa ambalo linazidi kuvuruga watu, nalo ni Uchumi (economics). Ndani ya uchumi kuna BIASHARA na masuala ya FEDHA. naomba kwa sasa nizungumzie upande wa FEDHA.
Kwa nini watu wanalalamika kila kukicha kuwa uchumi ni mgumu? Maisha ni magumu, wengine uongozi wa nchi ni mbaya hivyo umepelekea ugumu wa maisha. Unaweza ukaendelea kulalamika lakini hakutakusaidia hata kidogo.
Unalopaswa kujua ni hili: Mafanikio ya maisha yako ni wewe mwenyewe!
Watu wengi wanajua kuzalisha fedha, lakini idadi kubwa wanashindwa kujua kuwa kupata fedha nyingi iwe toka kwenye biashara au kazi hakutakufanya uwe tajiri hata siku moja. Ngoja nirudie tena! "Making more money every day does not make you rich! Tufahamu kuwa kuna tofauti ya kuingiza pesa nyingi na kufanikiwa sana. Ndiyo maana huwezi kushangaa kukuta mwenye kipato cha Tsh. 300, 000 kwa mwezi akiwa na mafanikio makubwa kuliko mwenye kipato cha Tsh.600, 000 kwa mwezi. 
Utofauti wao ni mtazamo wao wa kifikra juu ya misingi ya fedha. Ndugu msomaji umejiandaaje kuhakikisha unakuwa na mafanikio makubwa kiuchumi?

Hebu tujibu maswali yafuatayo:
1. Una vipaumbele katika maisha yako?
2. Una malengo ya muda mrefu katika maisha yako?
3. Ni lini umejiandaa kuingia kwenye orodha ya wenye mafanikio?
4. Ufanye nini ili utoke mahali ulipokwama kiuchumi?

Kama una vipaumbele jitahidi kuvitekeleza na kuhakikisha unafikia makusudi yako juu ya hivyo vipaumbele. Kama huna jitahidi uwe navyo, maana bila vipaumbele huwezi kuona mafanikio, sahau! Usiishi kama mbayuwayu, kumbuka tumeletwa duniani kwa makusudi fulani na baada ya muda sisi tunapita. 
Ngoja nikufikirishe jambo moja la muhimu: Siku moja nilikaa chumbani nikiwa na fedha mkononi mwangu, nikajiuliza swali lifuatalo: " Miaka 5 ijayo nitakuwa na umri wa miaka mingapi? Na katika umri huo natakiwa niwe nimeshafanya kipi na kipi? Je, watoto wangu watakapofikia umri X watakuta mazingira gani ya kiuchumi? Nilikaa kwa muda nikajisikia kutetemeka ndani yangu. Nilikumbuka fedha zilizopita mkononi mwangu, nikatoa machozi. Nilijiuliza jambo moja , nifanyeje ili niweze kufikia malengo yangu?
Siku moja nilikuwa nasoma makala moja iliyoandikwa na mzungu mmoja nikakuta neno hili "being poor is a decision and being rich is a decision too"
Maana yake "kuwa maskini ni uchaguzi na kuwa tajiri ni uchaguzi pia".
Baada ya kusoma hii sentesi nilijisikia vibaya sana nikajua huyu mzungu anadharau maskini. Lakini baada ya siku kadhaa nilimtembelea kaka yangu mmoja nikamuuliza hivi: Wengine wanafanyeje mpaka wanafanikiwa? Je, kuna ambao Mungu amewapangia kuwa masikini na wengine kuwa matajiri? Kaka akanijibu, hapana! Tofauti ya wanaofanikiwa na wasiofanikiwa ni kuwa wanaofanikiwa wanajua misingi ya fedha na wasiofanikiwa hawaijui. Akaendelea kusema hivi; "watu wengi wanafikiri kwa kuwa wana nguvu na wanaingiza fedha wanafikiri watakuwa matajiri automatically, lakini sivyo. 
Wakati naendelea kujifunza juu ya jambo hili nilibahatika kupata makala moja ambayo ilibadilisha maisha yangu.
Kama unataka kuona unaishi maisha ya uhuru wa kifedha fanya mambo yafuatayo: 
1. Hakikisha unajiwekea akiba.
Ndugu msomaji, haijalishi unapata fedha kiasi gani, tenga akiba kwanza kabla hujafanya matumizi yoyote. Watalaam wa fedha wanashauri angalau 15% ya pato lako liwe akiba.

2. Wekeza
Ndugu msomaji haijalishi unapata fedha nyingi au ndogo, wekeza fedha yako kwa watoao riba. Tafuta taasisi au kampuni nzuri na wekeza fedha zako huko. Wekeza kwa muda mrefu ndipo utaweza kupata faida kubwa. Hivyo, tenga kiasi kingine cha fedha kwa ajili ya kuwekeza.

3. Hakikisha una vitega uchumi zaidi ya kimoja.
Mifereji mingi ya fedha ni ya muhimu sana kwani mfereji mmoja ukikauka bado utaendelea vema kuliko kutegemea huo mmoja tu.

4. Uwe mtoaji (giving) kwa watu.
Utoaji ni kanuni moja ya kiroho ambayo ni ya muhimu sana kwa mwanadamu. tujitahidi kuwabariki wengine hicho tunachopata kwani kwa kupitia kwao tunapata zaidi wanapomtukuza Mungu. Huwezi kupokea kama hutoi.

kwa leo tuishie hapa. Somo lijalo tutaangalia hizi njia namna ya kufanya ili uweze kufikia malengo yako. Kila la heri rafiki yangu msomaji, wako master wa VIPAUMBELE KWANZA. Mungu akuzidishie kwa kila ulifanyalo.     

0 maoni:

Chapisha Maoni