Habari za jioni ndugu msomaji wa VIPAUMBELE KWANZA , pole na majukumu ya hapa na pale.
Binafsi sijambo namshukuru Mungu wa Mbinguni.
Jioni hii napenda kuzungumzia kwa nini watu wengi wanatamani kufanya biashara lakini huoni wakifanya hata siku moja. Mimi mwenyewe ni shahidi wa jambo hili. Nina marafiki ninaofanya nao shughuli za kila siku , utawasikia wakizungumzia biashara za kufanya mwisho wa siku unawaona wameahirisha kufanya. Ukiwauliza watakupa sababu za kila namna.
Sababu wanazotoa ni kama:
- Hawana mtaji
- Ni vigumu kupata mtu mwaminifu wa kufanya nao biashara
- Biashara hazitabiriki.
Hizi ni baadhi tu ya sababu za watu wengi kushindwa kufanya au kuanzisha biashara. Huwa najiuliza hawa watu wanataka biashara gani isiyoweza kupata hasara? Unajiuliza hawa watu wanahitaji kweli kufanya biashara au wanatania? Hivyo vyote ni visingizio tu.
USHAURI wangu kwako msomaji: Hata mimi hili jambo limenisumbua miaka michache iliyopita,
nilikuwa najiuliza biashara gani nifanye nitajirike fasta? Ni swali niliwauliza wengi sana, na waliniambia ni ipi japo nilikuja kugundua yafuatayo baada ya muda:
MOJA: Kwa nini watu wengi wanasingizia MITAJI katika kuanza biashara? Mimi nakiri wazi bila unafiki, anayeniambia hana mtaji huwa nakataa huu usemi, kwa sababu; unakuta mtu ana matumizi zaidi ya sh.130, 000/= kwa mwezi halafu ukimtazama ana simu ya laki 1 au zaidi, ukimcheki ana viatu vya gharama. Huyo huyo anakuambia hana MTAJI. Ukweli ni kwamba wengi wanatamani kuanza biashara kubwa kubwa zinazohitaji pesa nyingi. Na kwa sababu hiyo wanaishia kusema mtaji hautoshi na wengine huishia kuchukua mikopo ambayo mwisho wa siku inawaingiza katika madeni. Naomba nikushauri anza biashara ambayo unaweza kuimudi kimtaji. Usilazimishe kuanza biashara kubwa kubwa wakati hata ndogo hujawahi kufanya.
PILI: Kwa nini wengine wanasingizia biashara gani wafanye ya kuwalipa? Napenda kukueleza kuwa biashara zote zinalipa kutegemeana na mazingira biashara ilipo. Ishu sio biashara gani, ishu ni wapi biashara hiyo umeamua kuiweka tegemeana na mahitaji ya jamii. Cha msingi ni kuangalia mazingira, mahitaji ya jamii husika na ufanye utafiti wa kutosha ili ujue changamoto maana zipo. Lakini pia usisahau kuwa hakuna biashara isiyo changamoto.
TATU: Na kwa nini kuna kundi lingine husingizia kuwa UAMINIFU katika biashara ni mdogo. Ni kweli uaminifu ni changamoto inayowakabili wengi. Swali linakuja: Kama uaminifu hakuna au ni mdogo mbona idadi ya wafanya biashara inazidi kuongezeka kila kukicha? Kwa kuwa tunaishi na wanadamu hayo hayana budi kuwepo. Napenda nikiri kuwa huwezi kupata mtu mwaminifu kama unavyotaka, ukimpata ni bahati. Lakini hii haimaanishi kuwa hawapo, waaminifu wapo. Cha msingi ni kujitahidi kusimamia ipasavyo, usije ukamwachia biashara mfanyakazi wako (mwajiriwa). Jitahidi sana kuhakikisha unasimamia angalau kwa kiasi chake. Lakini pia usiogope kuibiwa visenti vidogo vidogo. Muhimu afanye biashara ilete faida.
NNE: Jambo lingine linalokwamisha wajasiriamali wachanga, ni kutokuwa na maandalizi ya kutosha kwa ajili ya malengo yao ya kuanzisha biashara zao. Kwa nini watu wanamatumizi makubwa lakini hawana mitaji? Ni kwa sababu wanakosa NIDHAMU YA PESA. Wanashindwa kuweka AKIBA kwa ajili ya siku zijazo ili iwasaidie kufanya biashara, wanajikuta wanatumia wanachokipata chote. Ukweli ni kwamba fedha yoyote huwa haitoshi, ndiyo maana wanashauri uweke akiba kabla ya matumizi.
TANO: Unapoona pia mtaji hautoshi, jaribu kuangalia watu gani uungane nao ili muunganishe mitaji yenu (kolabo) kwa kiswahili cha mjini. Ungana na wenzako muunganishe mitaji yenu mpate mtaji mkubwa ili muanzishe biashara mnayoitaka. Waswahili husema, KIDOLE KIMOJA HAKIVUNJI CHAWA.
Nawatakia jioni ya fanaka na Mungu awapiganie na kuwapa ujasiri. Zipo sababu nyingi lakini hizi chache zikupe changamoto zaidi. Wako katika VIPAUMBELE KWANZA blogu.
0 maoni:
Chapisha Maoni