Ndugu msomaji wa VIPAUMBELE KWANZA nakusalimu tena. Pole kwa shughuli za hapa na pale katika kujenga taifa letu.
Jioni hii nitazungumzia jambo moja kubwa nalo ni hili:
MAAMUZI JUU YA FEDHA UNAZOPATA KILA SIKU.
Ndugu msomaji nataka tuzungumzie ukweli juu ya jambo hili linalotukwamisha kila siku.
Swali nalotaka tulijibu wote jioni hii ni : Je, unapokuwa na fedha au pesa mkononi mwako huwa KWANZA unazitumiaje? Naamini kila mmoja wetu huwa ana maamuzi fulani juu ya pesa anazopata kila siku. Watu wengi wanafikiri kwa kuwa wana nguvu (energetic) wakati wanafanya kazi (while working) wanafikiri hiyo hali itaendelea kuwa hivyo. Nasema bila unafiki ndani yangu, siku zinabadilika. Kama makampuni makubwa yanafilisika si jambo la kushanga mtu mmoja akifilisika. Yapo mambo mengi yanayojitokeza hata ambayo hatukuyatarajia katika maisha yetu.
Tuache dhana ya kujisahau eti kwa kuwa napata pesa kila siku basi hakuna shida, huu ni uongo unaofanana na ukweli.
Hivyo ni jambo jema tukaishi kwa kuongozwa na utaratibu fulani katika matumizi ya fedha zinazopita mikononi mwetu. Tusije tukajikuta zimepita hela nyingi sana mikononi mwetu lakini tukajikuta bado tu masikini. Hujawahi kusikia watu wakisema "niliwahi kuwa na hela enzi hizo, sio sasa". Huu si ushuhuda mzuri kwa mwenye malengo mazuri ya kifedha katika maisha yake. Hakuna kitu kibaya unakuta mzazi anakwambia "mwanangu niliwahikuwa na hela kipindi cha ujana wangu usingeteseka hivi", ok ushuhuda kama huu unanisaidia nini mimi mtoto wake? Jibu ni rahisi , "ushuhuda kama huu hauna faida bali hukatisha tamaa maana inaonyesha wazi huyu mtu kuna namna ilitokea pesa ikapotea. Ni afadhali pesa ipotee kwa jambo ambalo ukilisikiliza lina sababu za msingi sio zile mbovu za kutumia pesa kama vile wewe ndo unayezitengeneza.
Pesa inayopita mkononi mwako usipoidharau inaweza kukufanya utajirike hata kama ni ndogo kiasi gani. Kutajirika si suala la wewe unapata pesa nyingi kiasi gani bali ni unaamua nini unapozipata hizo pesa. Unaweza amini kuwa mwenye kipato cha Tsh.300, 000 anajenga nyumba nzuri na mwenye Tsh.700, 000 anashindwa? Jibu ni rahisi na mifano mingi tunayo. Ushauri wangu kwako msomaji:
Unapopata fedha mikononi mwako, KWANZA tulia kabisa, pesa ni yako. Narudia tena, tulia kabisa kama vile huna hela. Baada ya kutuliza akili fanya yafuatayo.
Hatua ya kwanza: Tenga kiasi cha AKIBA kwa ajili ya baadaye. Wataalamu wa masuala ya fedha hutumia neno "pay yourself first". Wakimaanisha jilipe mshahara wako kwanza. Akiba hii usiiguse kabisa ni kwa ajili ya baadaye. Save for yourself for rainy day.
Jambo la pili: Tenga kiasi fulani kwa ajili ya KUWEKEZA.
Kiasi hiki si akiba ni fedha unayoirundika polepole kwa ajili ya kukuza mtaji ili siku utakapohitaji kuanzisha biashara usihangaike sana. Kama unafuatilia uchumi wa dunia unavyokwenda utakuwa unafahamu kuwa kadri siku zinavyokwenda, upatikanaji wa mikopo utakuwa wa masharti sana. Hivyo ni jambo jema sana ukiweza kujijengea nidhamu ya kifedha ili tusitegemee mikopo tu kama chanzo cha mitaji wakati pesa zinazopita mikononi mwetu ni nyingi.
Jambo la tatu: Fedha inayobaki ndo iwe MATUMIZI YALIYO YA LAZIMA.
Kumbuka kuna matumizi holela na matumizi yaliyo vipaumbele. Wengi tukipata fedha tunakimbilia kuweka kwanza matumizi ya kila siku, kisha ndo tunataka kuweka akiba kilichotuzidi. Hii inaweza kutumika kwa wale ambao walishajiweka vizuri kifedha. Kwetu sisi ambao bado tunaelekea kwenye mafanikio ni muhimu sana kufuata hizi kanuni za kifedha, financial management principles.
NB: Sijasema mikopo ni mibaya la hasha! Mikopo ni mizuri ukiitumia vizuri.
Muhtasari:
1. Weka akiba
2. Weka kiasi kwa ajili ya kuwekeza
3. Tenga matumizi yaliyo ya lazima. Kumbuka: Usiweke AKIBA kinachobaki. Haya niliyoyaandika yamenisaidia na mpaka leo nayatumia.
Nawatakia mafanikio mema.
0 maoni:
Chapisha Maoni