Ijumaa, 24 Februari 2017

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA NDOA YAKE KIBIBLIA

Bwana Yesu asifiwe mpendwa msomaji! Tumsifu Yesu Kristo!
Naamini unaendelea vizuri katika kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani..Na ninaamini unaendelea kujitakasa katika Bwana ili ajapo kulichukua 'kanisa lake takatifu' na wewe uwemo, haleluya!
Ndugu msomaji napenda kukushirikisha jambo hili muhimu la NDOA katika kizazi hiki. Ukitazama makanisani, katika jamii, maofisini,n.k. suala la migogoro ya ndoa limekuwa jambo la kawaida. Siku hizi hata "watu wale wa njia hii" nao kuachana au kupeana talaka limekuwa jambo la kawaida sana. Wakati umefika ambapo kila aliye wa Bwana ijulikane! Tumesahau kuwa sisi wa Ulimwengu huu, na shetani amepofusha wanandoa kwa kuwa hawazijui nafasi ambazo Mungu amewapa ili waweze kutimiza kusudi lake jema! Ukifuatilia Biblia kwa msaada wa Roho Mtakatifu, utagundua kuwa suala la NDOA mwanamke amepewa nafasi zake na mwanaume amepewa nafasi zake kiroho ili kuhakikisha ndoa inatimiza kusudi lake. Leo napenda nikushirikishe nafasi mojawapo ya mwanamke katika ndoa. Kibiblia mwanamke amepewa nafasi (positions) nyingi za kumsaidia kuimarisha NDOA YAKE. Nafasi hizo ni kama ifuatavyo:

Mwanamke kama Mjenzi kwa mumewe
Mwanamke kama Msaidizi
Mwanamke kama Mleta Kibari kwa mumewe
Mwanamke kama Mshauri wa mumewe
Mwanamke kama Mlinzi kwa mumewe n.k.

Ndugu msomaji, unajua kuwa mwanamke akisimama kwenye nafasi yake amepewa "mamlaka" ya kujenga ndoa yake? 
Hebu tusome (Mithali 14:1) kwa pamoja. 
"Kila mwanamke aliye na "hekima" hujenga nyumba yake;Bali aliye "mpumbavu" huibomoa kwa mikono yake mwenyewe".
Haleluya! Biblia inasema, "mke mwenye hekima ndiye anayejenga nyumba yake, tena kwa mikono yake mwenyewe. Lakini pia inasema, mke mpumbavu anbomoa nyumba yake...Neno "nyumba" linaashiria "familia" au "ndoa". Sikia mtu wa Mungu, mwanamke amepewa nafasi au wadhifa katika ulimwengu wa Roho kujenga nyumba yake au ndoa yake au familia yake. Hii haimaanishi 'baba' hana nafasi katika ndoa yake, hapana; isipokuwa katika somo hili nazungumzia mwanamke (woman). Ikiwa kina mama wataamua kukaa katika nafasi zao, ukweli ni kwamba ndoa zitapona. Kanisa litaimarika, utukufu apewe Yesu Kristo! "mpumbavu" ni mtu yule anayejua anachopaswa kufanya lakini hafanyi. Biblia haisemi "mwanamke aliye mjinga" bali "aliye mpumbavu". Sikia mama neno hili ambalo Roho anakukumbusha, keti katika nafasi yako katika ndoa yako, na nafasi mojawapo ni KUIJENGA NYUMBA YAKO, kumbuka kuwa kama kuna suala la kujenga, uwe na uhakika, si suala la siku moja, bali ni suala la kila mara panapotokea ufa.
NB: Huwezi kujenga nyumba ambayo imekamilika, bali unajenga nyumba ambayo haijakamilika. Hivyo hekima yako inahitajika mama hasa pale "ndoa yako inapokuwa katika changamoto" ili ujenge mahali penye nyufa. 

Mambo unayopaswa kuzingatia ili uweze kujenga nyumba yako (ndoa yako).

1. Utiifu kwa mumeo
Sikia ewe mwanamke, maandiko yanatuambia kuwa; mnapaswa kuwatii waume zenu kama kumtii Bwana.
Ukisoma Waefeso 5:22, "Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu".
Ili mwanamke aweze kujenga nyumba yake hana budi kumtii mumewe, tena amtii kama vile anavyomtii Bwana Yesu wetu Kristo. Hili si jambo dogo, ni jukumu kubwa lakini lenye baraka na ushindi kwenye ndoa na Ufalme wa Mungu. Kwa nini siku hizi kina mama walio wengi hawataki kuwatii waume zao? Wanategemea kweli ndoa zao zikae salama wakati mioyo yao imejaa dharau, kiburi na visasi visivyoisha? Ndivyo neno la Bwana linavyotufundisha? Sikia mwanamke jambo hili, haijalishi mumeo anakufanyia vituko gani, ikiwa kweli Bwana Yesu ni tegemeo lako, hutajaa dharau na kiburi kwa mumeo. Wewe unachopaswa kufanya ni kuonyesha kuwa unamtii tena kama kumtii Bwana wetu Yesu. Soma 1Petro 3:1. "Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno".
Umeona mwanamke unapokuwa mtiifu kwa mumeo kinachotokea? Maandiko yanasema, "mwenendo wa mke ukiwa vizuri; unaweza kumvuta hata mume asiyeamini, halelujah! Mume wako akigundua unamtii toka moyoni mwako pasipo unafiki, nakueleza ukweli, utashangaa kitakachotokea. "Utii wako ni mbinu mojawapo ya kuijenga ndoa yako mama. Usikubali Ibilisi akudanganye na hila zake, wewe mtii mume wako. Kumbuka kuwa "usipomtii mumeo" unatenda dhambi. Utaniuliza kwa nini? Kwa sababu "dhambi ni uasi"(1Yohana 3:4). Kwa lugha nyingine, unaasi maagizo ya Mungu katika neno lake la kuwa "umtii mume wako". Maandiko hayasemi umtii mume anayemwamini Bwana wetu, bali hata kama hamchi Mungu wewe "mtii tu". Mungu akutie nguvu katika Kristo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu ili akupe nguvu na hekima uweze kujenga ndoa yako. Biblia inasema, "Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu (Wafilip 4:13). Sikia mwanamke, hata wewe unayaweza mambo yote katika yeye akutiaye nguvu.

2. Kutunza siri za mume wako.
Je, huwa unatunza siri za mumeo ewe mwanamke? Kwa nini hufanyi hivyo? Miongoni mwa vitu ambavyo Ibilisi anatumia ni "kina mama kumpa nafasi katika kutoa siri za waume zao nje wakidhani watasifiwa au kusaidiwa. Sikia mama na uelewe, haijalishi mumeo ana mapungufu kiasi gani, usiyatoe nje, yatunze kwani huo ni udhaifu tu wa mumeo. Usitumie udhaifu wake kumpiga nyundo kichwani, bali tumia udhaifu wake kumjenga na kumuombea. Sijaesema kuwa usitafute msaada kwa wapendwa, hapana, ila Roho akuongoze kwa mtu ambaye ana hekima ya Mungu, bali si kila mtu unamueleza mambo ya ndoa yako, linda kinywa chako uwe na siri. Narudia tena, tunza siri za mume wako hata kama anakutesa. Sisi si wa ulimwengu huu, na wewe si wa ulimwengu huu, hivyo, mienendo ya ulimwengu huu haikuhusu (Yohana 17:16). 
Ukisoma "Tito 2:3-5), neno la Mungu linasema hivi:
"....ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao, na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe"
Nataka uone hili neno, "kuwa wenye kiasi" "self-control" . Sikia mwanamke, jitahidi usiseme mambo ya ndoa yako, maandiko yanasema, uwe na kiasi katika uyatendayo yakiwemo na ya mumeo. Unafikiri unapopeleka siri za mumeo nje unamsaidia? La hasha! humsaidii bali unatoa nfasi kwa shetani ili aweze kuwavuruga. Mpende mumeo na umuombee....Be self-controlled in all you do. 

3. Matumizi ya kinywa chako
Miongoni mwa viiungo Ibilisi anavitumia kuangamiza watoto wa Nuru ni 'vinywa vyao' au maneno ya vinywa vyao yasiyo na uzima ndani yao wanayoyatamka juu ya waume zao bila kujua madhara yake. Hebu tusome (Mithali 18:7-8). "Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake mwenyewe, na midomo yake ni mtego wa nafsi yake". Maandiko yanasema, maneno yanayotoka kinywani mwa mpumbavu huharibu nafsi yake, na maneno hayo ni mtego wa nafsi yake. Jizuie usimnenee mumeo maneno mabaya, kwani yeye (mume) ni kichwa chako. Tusome pia "Zaburi 36:4, Huwaza maovu kitandani pake, hujiweka katika njia mbaya; ubaya hauchukii". Ukisoma kwa makini mstari huu, utaona jambo hili. Mpumbavu anaponena bila utaratibu hujiweka katika njia ya uangamivu, na mtu wa namna hii hachukii hata ubaya. Kumbuka jambo hili, kuna roho za giza ambazo zinafuatilia maneno unayosema juu ya mumeo ili yaumbike na unashangaa yanampata. Mungu amekupa nafasi uzitumie kujenga na si kubomoa. Haijalishi mumeo yukoje, wewe mnenee mema kila wakati. Laiti watu wangejua uharibu unaotokana na maneno ya vinywa vyao, naamini wangelinda sana maneno yawatokayo. ukisoma (Mithali 12:14a "Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake.....
Siku zote mtu hujazwa na yale asemayo kutoka kinywani mwake. UKISOMA Mithali 12:22a, "Midomo ya uongo ni chukizo kwa BWANA......Ukisoma ule mstari wa 18, Biblia inasema, kuna kunena bila kufikiri....Jitahidi kabla hujanena ufikiri unachotaka kusema juu ya nyumba yako au ndoa yako. Acha umbeya wewe si wa ulimwengu huu (Yohana 17:16), tena ya kale yamepita sasa yamekuwa mapya (2Kor 5:17). Soma Mithali 13:3, "Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu. Linda kinywa chako mama ili uilinde nafsi yako na uepuke uharibifu. Ombea kinywa chako na ukikabidhi kwa Bwana ili kitumike kama silaha ya haki.

4. MSAMAHA
Biblia inasema, kabla mtu hajaomba hana budi kwanza kusamehe waliomkosea. Marko 11:25, 26. "Nanyi kila msimamapo na kusali, SAMEHENI MKIWA NA NENO JUU YA MTU; ili na Baba yenu aliye mbinguni AWASAMEHE ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehi, wala Baba yenu aliye mbinguni HATAWASAMEHE ninyi makosa yenu". 
Mungu atusamehe wapendwa, eneo hili ni la muhimu sana. Mimi naamini kuwa, mtu akiweza kuwa na roho ya kusamehe; huyo atashinda vikwazo vingi na atakuwa na AFYA NAFSINI mwake siku zote. Ukisoma hayo maneno juu utaelewa jambo hili: Ukitaka maombi yako yasikilizwe na Baba yetu wa Mbinguni ni lazima "tuwasamehe" waliotukosea. Lakini pia, tusipowasamehe, tunatenda dhambi kwa sababu tumeasi maagizo ya Mungu. Na dhambi ni uasi 1Yohana 3:4. Hivyo huwezi kuitwa tena mwana wa Mungu. Ukisoma hii mistari vizuri, haisemi tuwasamehe wakituomba msamaha la hasha! Tunatakiwa kusamehe bila kuombwa msamaha. Wanawake wengi siku hizi za mwisho, atakuambia; "nimemsamehe mpaka nimechoka". Unakumbuka wanafunzi wa Yesu walivyomuuliza Yesu "mtu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu aliwajibu sikuambii hata mara saba bali hata saba mara sabini...wanafunzi wakamjibu, Bwana tuongezee imani. Hivyo, Yesu alikuwa anawafundisha kuwa, wasamehe hata bila kuombwa msamaha. Haijalishi unakosewa mara ngapi kwa siku wewe samehe. Kibaya zaidi, wake pasipo kujua nao wanalipa visasi dhidi ya waume zao. Usilipe kisasi ewe mwanamke, kisasi ni cha Bwana yeye atalipa. Mume wako akikosea wewe mbebe kwenye maombi. Najua utanimbia, "nimeomba mpaka nimechoka, ni sawa kwa jinsi ya kibinadamu; lakini kwa jinsi ya Rohoni, hutakiwi kuchoka. Soma (Yakobo 5:10-18, Mathayo 5:14).
Ufanye nini ili usamehe mume wako? Fanya yafuatayo:
Moja: Fahamu kuwa si wewe bali Kristo aliye ndani yako. Wagalatia 2:20. Ukifanyiwa mabaya hufanyiwi wewe bali Kristo aliye ndani yako.Mume wako akikutukana; wewe linda kinywa chako huku ukijua kuwa hutukanwi wewe bali Yesu aliye ndani yako. Ukipigwa, usirudishe bali fahamu kuwa anafanyiwa hayo Yesu aliye ndani yako. Kusameheana hakupo siku hizi kati ya wanandoa, kwani upendo wa wengi umekwishapoa. 

Pili: Mpende mume wako (adui yako) na umuombee.
Mathayo 5:43, 44. MMesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako na umchukie adui yako; Lakini mimi (Yesu) nawaambia, wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi. Jizoeze kumuombea mume wako anapokuudhi. Tena mpende hata akikufanyia ubaya. Kumbuka kila wakati jambo hili muhimu, hakuna msamaha wa kweli pasipo upendo. Yohana 3:16.
 Watu wengi wanafanya kile Yesu alichowaambia wasifanye..Yesu alisema "wapendeni adui zenu".Kama adui unatakiwa umpende, kwa nini unamchukia mume wako? Katika watu wa Mungu, chuki imejaa na hii imeharibu ndoa nyingi. Biblia inasema, tuwapende wale wanaotuudhi. Kwa nini Yesu alisema tuwapende wale wanaotuudhi? Ni ili tupate kuwa wana wa Baba yetu (Mungu) Mathayo 5:45-47.ukisoma 1kor 13:4-8, utakuta tabia za upendo wa watu wa nuru. utakuta uvumilivu, kustahimili yote, kuamini yote, upendo haupungui wakati wowote, hufadhili, hautakabari, hauhesabu mabaya, hauoni uchungu n.k. 
 
Tatu:  samehe na kusahau
Ukisoma 'Luka 17:4, 5.  Maandiko yanatuambia, ...hata saba mara sabini, maana yake hata usipoombwa msamaha wewe samehe. Kusamehe ni uamuzi wa mara moja lakini kusahau ni vita vya imani. Ngoja nikuulize swali, Je! siku ulipookoka ulikuwa na uhakika gani kuwa umesamehewa dhambi zako na wala Mungu hazikumbuki tena? Lakini je, unaona kuwa Mungu anaweza kukuambia ufanye kitu aambacho anajua huwezi kufanya? Kumbuka ukimsamehe mume wako, usikumbuke tena hayo na usiyaweke moyoni. Msamehe bila unafiki ndani yake. Haleluya! haleluya! Tunayaweza mambo yote....Wafilipi 4:13. Soma pia Yakobo 4:7, Waefeso 4:27, Wafilipi 4:8. Kumbuka unasamehe kwa ajili yako mwenyewe.

Nne:Peleka hasira kwenye maombi
"Mwe na hasira, ila msitende dhambi jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi" (Waefeso 4:26-27). Huu mstari wa "mwe na hasira ila msitende dhambi" watu wameutumia isivyo. Kutokana na maneno hayo wamefanya vitendo vingi viovu kwa mawazo, maneno na kwa matendo. Biblia haiwezi kujipinga yenyewe. Roho Mtakatifu ndiye aliyewaongoza watu kuandika maandiko hayo matakatifu. Lakini, soma mistari ifuatayo: 
"Uchungu wote na gadhabu na HASIRA na kelele na matukano YAONDOKE KWENU" (Waefeso 4:31). 
.....HASIRA ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu" (Yakobo 1:20).
"Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya HASIRA na watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu (Wagalatia 5:19-21). Hapa unaona jinsi hasira inavyofananishwa na uchawi, uasherati, uadui, ibada ya sanamu, na mambo mengi yanayofanana na hayo.
Ukisoma (Mathayo 5:21, 22), Yesu akikaza ubaya wa hasira alisema "Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, kila amwoneaye ndugu yake HASIRA itampasa HUKUMU". Yesu anasema ukimuonea ndugu yako hasira unastahili hukumu...lakini Roho aliyema ndani ya Paulo ni huyo huyo aliyesema ndani ya Yesu. Tukirudi kwa Paulo, maandiko yanasema, ikitokea ukakasirika kwa sababu ya maudhi, jitahidi usitende dhambi. Maadamu tupo chini ya jua, hatutaweza kukwepa kukasirika, lakini Roho anasema kuwa "tukikasirika tusitende dhambi". Hivyo kuwa na hasira ni dhambi, ndiyo maana Yesu anasema, ukimwonea hasira ndugu yako (mume wako) unastahili hukumu, yaani umefananishwa na muuaji, mwasherati, mwabudu sanamu na mambo kama hayo. Swali linakuja, ikiwa umekasirika ufanyeje? Nakushauri katika Roho wa Mungu, fanya yafuatayo...
1. Kwana tubu kwa Baba juu ya kukasirika kwako
2. Pili, mwambie Baba jinsi unavyojisikia moyoni mwako bila kumficha kitu.
3. Tatu mwombe kitu ambacho ungependa akufanyie, utajikuta unaumimina moyo wako kwa Bwana naye ataichukua hasira yako na uchungu uliokuwa nao. Na badala yake anahuisha upya upendo ndani ya moyo wako. Ukiona bado hasira inakusumbua "ikemee kwa jina la Yesu nayo itatoka. Kosa la wengi wakiudhiwa wanapeleka uchungu na hasira kwa aliyewaudhi, sivyo biblia inavyoagiza, wewe upeleke kwenye kwa Yesu kwa njia ya maombi.

Tano: FURAHI SIKU ZOTE
Siri ya ushindi katika matatizo yoyote inatokana na furaha ya Bwana ndani yetu. Furaha ya Bwana ndiyo nguvu zetu. Wafilip 4:4;Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema, Furahini. 
Ndugu msomaji Bwana na akubariki, akupe macho ya ndani uone kile anachotaka ukione, hakuna ndoa isiyo na mapungufu, lakini Yesu alitununua ili tujenge boma, na wewe mwanamke, tumia nafasi hii ya KUJENGA ili ujenge ndoa yako. Kumbuka iko mikononi mwako. Mungu awabariki, nawatakia Jumamosi njema.             

 

Maoni 23 :

  1. Mungu akubariki sana kwa somo zuri

    JibuFuta
  2. Barikiwa sana kwa somo zuri..

    JibuFuta
  3. Ubarikiwe saana kwa maneno ya hekima kwa wanna ndoa

    JibuFuta
  4. Majibu
    1. Asante sana sanakwa somo zuri

      Futa
  5. Somo zuri BWANA Yesu akubariki

    JibuFuta
  6. Nimebarikiwa sana๐Ÿ™๐Ÿ™

    JibuFuta
  7. Ahsante sana. Barikiwa!

    JibuFuta
  8. Somo limeniponya barikiwa

    JibuFuta
  9. Mungu akubariki sana kwa mafunzo mazuri

    JibuFuta
  10. Mungu akubariki

    JibuFuta
  11. Mafundisho haya yananifanya niende kiwango kingine leo la kukutenda MUNGU atajua asante

    JibuFuta
  12. Mungu akubariki

    JibuFuta
  13. Mungu akubariki kwasomo zuri

    JibuFuta
  14. Somo nimelipenda sana barikiwa sana

    JibuFuta
  15. Mume wangu amerudi!!! Baada ya miaka 1 ya ndoa iliyovunjika, mume wangu aliniacha na watoto wawili na maisha yangu yalivunjika. Nilitaka kuyamaliza, nusura nijiue maana alituacha bila chochote. Nimekuwa nimevunjika kihisia wakati huu wote na maisha yanaonekana kutokuwa na maana. Siku moja mwaminifu, nilipokuwa nikivinjari mtandao, nilikutana na baadhi ya shuhuda kuhusu Dk DAWN. Baadhi ya watu walishuhudia kwamba alimrudisha mpenzi wao wa zamani, wengine walishuhudia kwamba anarejesha tumbo na kuponya magonjwa kwa mimea. Nilipendezwa zaidi na upatanisho na mume wangu, ambao Dk. DAWN aliwezesha kumrudisha mume wangu ndani ya siku 3. Sasa mume wangu amerudi na tumekuwa tukiishi kwa furaha tangu wakati huo. Shukrani zote kwa Dk DAWN. Hapa, ninaacha mawasiliano yake kwa kila mtu. Maana kuna changamoto za aina yoyote,
    Barua pepe ( dawnacuna314@gmail.com )
    Whatsapp: +2349046229159

    JibuFuta
  16. Maneno mazuri sana

    JibuFuta
  17. Kwenye masikio na asikie

    JibuFuta
  18. Mungu akubariki mtumishi wamungu ameni

    JibuFuta
  19. Barikiwa sana

    JibuFuta
  20. Be blessed

    JibuFuta