Jumatatu, 6 Machi 2017

MAISHA YAKO YANATOKANA NA UNAVYOWAZA NDANI YAKO

Habari za Jumatatu rafiki yangu! 
Naamini unaendelea vizuri na harakati za kujikwamua kimaisha kila siku. Leo nataka nikushirikishe jambo moja muhimu nalo ni "kiwango cha maisha ya mtu kinatokana na kiwango cha mawazo yake". Huu ni ukweli usiopingika ukiamua kujifanyia tathmini wewe mwenyewe. Kwa lugha nyingine, yale anayoyawaza mtu ndiyo atakayoyatenda na kuyaishi. Kuna msemo usemao, "you are what you eat". Hata kimawazo, mtu anaishi kwa kutekeleza mawazo anayoyaona kuwa kwake ni sahihi. Mawazo ni nini? Mawazo kwa tafsiri isiyo rasmi ni mtazamo alionao mtu juu ya jambo fulani au kitu fulani na kuamini kuwa ndivyo kilivyo.
 Mawazo haya yanatoka wapi?
Mawazo yanayomwongoza mtu yanatokana na vyanzo vingi. Yanaweza kutokana na anapokuwa anajifunza jambo. Kwa mfano, mtoto ukimwambia kuwa usipokuwa msafi utapatwa na magonjwa mbalimbali, mtoto huyo atapata mtazamo mpya ndani yake kuwa uchafu huleta magonjwa, na akilifanyia kazi wazo hilo ndivyo atakavyoishi.

Chanzo kingine cha mawazo ni yale anayoyasikia na kuyaamini kuwa ndivyo 
yalivyo.
Mtu huyu ataanza kutekeleza katika maisha yake yale yote aliyoyasikia na ndivyo atakavyoishi.

Chanzo kingine ni yale anayoyasoma kwenye maandiko mbalimbali yawe ya kidini au ya kawaida.
Ndiyo maana kwa urahisi zaidi angalia misimamo ya watu juu ya imani za dini zao. Hawa watu wanaishi na kutekeleza kile kilichoandikwa na ndiyo maisha yao yanakuwa katika wigo wa kile wanachokiamini.
Kwa mfano niliwahi kusikia mtu mmoja akisema kuwa kufanya kazi kwa bidii ni kutokuwa na imani, huyu mtu kamwe hawezi kuishi kwa kujishughulisha katika maisha yake.

Hivyo muonekano wa nje wa mtu ni matokeo ya yale anayoyawaza ndani yake. Kwa mfano siku moja nikiwa kazini kwangu tulikuwa tunabishana na wafanyakazi wenzangu juu ya utajiri na umaskini.
Swali lililoibua mjadala lilikuwa hivi:
"Kitu gani kinamfanya mtu mmoja awe tajiri na mwingine awe masikini? Je hawa watu wamepangwa na Mungu waishi hivi?
Hili ndilo swali lililoibua mjadala. Watu waligawanyika pande mbili zinazopingana, upande wa kwanza wanaamini kuwa, ukiwa masikini ujue umeumbwa uwe hivyo tena walisimamia mstari wa Biblia wa "Mithali 22:2, unaosomeka hivi:Tajiri na maskini hukutana pamoja; Bwana ndiye aliyewaumba wote". Ni kweli ukitazama haraka huu mstari unaweza ukakubaliana nao, lakini ukitafakari kwa kina hutakubaliana nao, kwa kuwa wao wanauelewa isivyo. Nasema hivyo kwa sababu ukisoma 2Wakorintho 8:9, Biblia inasema hivi: "Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake".
Ukisoma vizuri hapa utaelewa kuwa Yesu alipokuja duniani na Ufalme wake mabegani mwake, mojawapo ya vitu alivyokuja kufanya ni kugongomelea laana ya umaskini msalabani, ili sisi tuwe matajiri. Alibeba umaskini tuliokuwa nao ili tupate neema upya ya kuwa matajiri.
Baada ya andiko hili mjadala ulipamba moto, ikabidi niwapeleke kwenye maandiko haya, Isaya 48:17 " Bwana Mkombozi wako, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye katika njia ikupasayo kuifuata".
Baada ya andiko hili wakasema tumekuelewa kwa kiasi fulani. Kwa nini walinielewa? Kwa sababu Biblia haijipingi, bali inafafanua jambo kwa vifungu vingi, ndiyo maana si vizuri kusimamia mstari mmoja.
Kama Mungu ndiye atupaye nguvu ili tupate faida, inawezekanaje wengine awaumbe maskini? 
Ukisoma kwa kingereza andiko walilosimamia utaelewa vizuri, maana inasema, maskini na tajiri wote waliumbwa na Mungu na wanaishi wote katika dunia hii moja. Biblia haijasema, ALIWAUMBA MASKINI NA MATAJIRI. Sasa tuyaache hayo turudi kwenye somo letu. Baada ya hapo waliniuliza hivi:
Sasa wewe unafikiri ni kwa nini iwe hivyo?
Niliwajibu hivi: Utofauti wa maisha yetu ni kuwa na FIKRA TOFAUTI juu ya namna ya kufanikiwa. Niliwaeleza kuwa vile unavyojua kitu ndivyo unavyokifanya si zaidi ya hapo. Kama umefundishwa baiskeli huwezi ukaendesha gari bila kujifunza gari. Niliendelea kuwaambia hivi, akili ya mtu ili iweze kuishi vizuri lazima ipate mafundisho sahihi. Niliwapa mfano, mtoto ukimfundisha "kuhesabu" 1, 2, 3, 4....ukamwacha. Hawezi akajua kusoma moja kwa moja (automatically) kwa kuwa tu anajua kuhesabu. Lazima pia afundishwe kusoma ndipo ataweza kusoma. 
Vivyo hivyo na watu wazima kuna vitu tusipofundishwa hatuwezi kuvijua. Ndiyo maana wasomi kuwa maskini si suala la kushangaza, kwa kuwa mifumo ya elimu ya nchi nyingi hazimuandai mtu kufanikiwa kimaisha bali zinamuandaa mtu awe mtaalamu wa kile anachosomea tu. Hivyo ili msomi naye afanikiwe inabidi apate mawazo mapya yanayohusu mafanikio. Ndiyo maana na kuna mtu ukimpa mil30 bado ataendelea kuwa maskini pamoja na kuwa na hela zote hizo.
Mimi mwenyewe kuna siku nilikuwa natafuta kitu kwenye GOOGLE nikakutana na neno linasema hivi:
Learn to save in whatever little you earn. Kwa mara ya kwanza nilianza safari ya kuweka akiba. Lakini nilikuwa nikiweka akiba najikuta nimeitumia. Siku moja nikakuta kitabu kimeandikwa, the decision you take on the money in your hand, can make you rich or poor.
Baada ya kusoma hicho kitabu maisha yangu na mtazamo wangu juu ya pesa umebadilika kiasi fulani.
Ushauri wangu kwako. Jifunze na jizoeze kusoma vitabu mbalimbali vinavyohusu mafanikio unayohitaji. Lakini uwe mwangalifu na vitu unavyosoma, maana kuna falsafa nyingine ambazo ukitaka kuweka kwenye matendo vitu haviendi. La msingi mwombe Mungu akusaidie kabla hujasoma kitabu au makala yoyote maana si vyote ni vya kusoma. Kuna maandiko unaweza ukasoma na maisha yako yakawa mabaya.
Tumia muda wako kujifunza zaidi kwani akili yako inahitaji kupata maarifa mapya. Kumbuka hivyo ulivyo ndivyo unavyowaza ndani yako.
Nakutakia kila laheri rafiki yangu. Wako mwandishi na refarii wa VIPAUMBELE KWANZA.
 
 



 

0 maoni:

Chapisha Maoni