Ni matumaini unaendelea vizuri na umeamka salama katika siku hii njema. Binafsi namshukuru Mungu wa Mbinguni kwa neema hii aliyotukirimia siku ya leo.
Ndugu rafiki, naomba tujiulize swali hili muhimu: Kwa nini imekuwa ni kitu cha kawaida kwa watu wengi kuwa ni mipango lukuki kila mwanzo au mwisho wa mwaka, lakini cha kushangaza zaidi ni kuona watu wakiishia kulalamika kuwa mipango waliyopanga imefeli yote, tatizo liko wapi? Tatizo ni nini hasa?
Watu walio wengi hupanga kuanzisha biashara lakini huoni wakifanya hivyo hata kama fedha wanazo, kwa nini?
Kuna rafiki yangu mmoja alinipigia simu, akitaka ushauri wa kuchukua mkopo ili anzishe biashara, na mimi kabla ya kumshauri nilimuuliza maswali kadhaa. Na baada ya kumuuliza alinieleza kuwa, amekuwa akipanga kufanya biashara lakini kila akipata hela au pesa matatizo au changamoto huibuka toka kila kona, na mwisho wa siku ni kuahirisha hiyo biashara. Aliongeza kuwa changamoto kubwa kwake ni kutegemewa sana na familia yao.
Kiukweli alichosema nilimuelewa vema, lakini tuamue kuishi hivi kwa kuwa tu tunategemewa? La hasha!
Nilimuambia hivi, japokuwa unatamani kuwasaidia ndugu zako, kuna siku utashindwa kabisa na utajikuta umeingia kwenye madeni yasiyokoma! Soma pia umekwamishwa na nini rafiki?
Ndugu msomaji nakuomba tufuatane hatua kwa hatua, kwa nini watu wengi wamekuwa na maneno tu basi huku wakilaumu kwa nini wameshindwa biashara.
Wanapopata fedha za kuanzisha biashara zinawavuruga.
Kuna watu hawawezi kukaa na fedha nyingi mfukoni mwao, utadhani zinawawasha, utakuta wanatapanya fedha ovyo hovyo, huku wakinunua vitu ambavyo hata havina uhitajiwa. Watanunua simu kubwa na za gharama huku wanazo nyingine, watanunua mavazi huku wanayo ya kutosha, wataponda starehe za kila namna, baada ya fedha zao kuisha ndipo wanashtuka na kugundua hawajafanya lolote. Kundi la namna hii lipo. Ndugu msomaji wa makala zangu, nakushauri uajizoeze kuwa na nidhamu ya fedha zako, kumbuka kitakachokufanikisha kimaisha si kuwa na fedha tu mkononi au kwenye akaunt zako, la hasha! bali ni maamuzi sahihi utakayokuwa unachukua katika kutekeleza vipaumbele vyako vilivyo bora. Kumbuka si vipaumbele vyote vya mtu ni bora, vinginevyo kila mtu angekuwa na maisha mazuri.Narudia tena, heshimu fedha unazopata ziwe ndogo au nyingi.
Jambo lingine linalowakwamisha wengi ni kukosa uamuzi wa kutosha na yakini ndani yao.
Nadhani unafahamu kuwa kuna watu ni wepesi kusema chochote popote walipo ili mradi wasikike wamesema. Watu wa namna hii utawasikia wakisema, mwezi ujao lazima nianzishe mradi wa X .
Sijui wanatafuta sifa au waonekane wanajua kupambana na maisha au la! Ndugu msomaji, hutaanza biashara yoyote kama hujaamua kweli toka moyoni mwako. If you are really committed, hakuna cha kukuzuia kufanya biashara. Amua kuwa nataka kufanya biashara tena wekaa na muda, usipende kuahirishaahirisha kila siku, kumbuka siku hazirudi nyuma. Usipoteze muda wako, chukua hatua fanya biashara hata kama ni ndogo.
Jambo lingine baya zaidi linalowakwamisha watu wengi wasiaanzishe biashara ni "woga".
Hivi unaogopa nini mwenzangu? Mbona vitu vingine huogopi kuvifanya? Unaogopa nini? Hofu, hofu, hofu, hofu ndo vimejaa kwa watu. Wanaogopa kuanzisha biashara utadhani kuna mkono wa mtu. Kama una woga kemea hali hiyo kwa Jina la Yesu na itatoka.
Vunja woga iliyo ndani yako, usijihukumu mwenyewe kuwa hufai kuanzisha biashara wanaoweza ni watu fulani tu..Si kweli, kila mtu anaweza kufanya biashara, kadri unavyofanya ndivyo unavyojifunza zaidi, waingereza wanasema, "There is no school of experience", wakimaanisha kuwa, hakuna shule ya kufundisha uzoefu. Nakushauri kuwa ONDOA HOFU NDANI YAKO.
Jambo lingine linalozuia watu kuanzisha biashara ni ukosefu wa akiba.
Watu wengi wanatamani kuanzisha biashara au shughuli mbalimbali, lakini wanajikuta hawana fedha, na kwa sababu hiyo wanakwama kufanya walichokikusudia kufanya. Jizoeze kuweka akiba rafiki yangu kwa kuwa hii itakusaidia utakapohitaji kufanya biashara. Na hii inawafanya wengi kujikuta wameingia katika kuchukua mikopo inayowagharimu. Ningeshauri hivi, kabla hujachukua mkopo wowote, anzisha biashara kwanza ujipime na ufanye utafiti wa biashara yako ndipo sasa unaweza kukopa mahali.
Kitu kingine kinachozuia watu wengi ni kutamani kuanzisha biashara kubwa.
Ndugu rafiki yangu, jitahidi sana kutokimbilia kuanzisha biashara kubwa wakati unaanza kwa mara ya kwanza. Anza na kidogo, ili ujue changamoto za biashara yako, ili ujifunze kipi kinahitajika zaidi na kipi si cha lazima katika biashara yako, endelea kujifunza zaidi ili ujue namna ya kukuza biashara yako, ukishaijua biashara yako inavyotakiwa kuendeshwa unaweza ukaongeza mtaji wako na kupanua biashara hiyo. Usimbilie biashara kubwa wakati hata ndogo hujawahi fanya. Wengi imewaumiza na kuna wengine hata hamu ya biashara imetoweka ndani yao. Wamekwama jumla kwa kuwa walipoianza walijua ndo mafanikio tayari, kumbe kuna muda wa kujifunza kuhusu nini kinatakiwa, kipi kinaweza kuikwamisha, changamoto zake na mambo kama hayo. Rafiki nikushauri, anza na kidogo kwanza.
NB: Maskini akipata hela husema hivi, "ninunue kitu gani cha thamani"?
Tajiri akipata hela hujiuliza hivi, "nianzishe mradi gani unizalishie fedha zaidi"?
Umeona hii tofauti kati ya maskini na tajiri au mjasiriamali? Jifunze kitu kutoka hapa! Nakutakia Jumamosi ya fanaka katika shughuli zako! Wako refarii wa VIPAUMBELE KWANZA "Faustine Mahende".
0 maoni:
Chapisha Maoni